Wimbo wa Beyonce wa Brown Skin Girl uliopo kwenye albamu yake, The Lion King: The Gift ambao kawashirikisha Blue Ivy, Saint JHN na Wizkid ulishinda katika kipengele cha Best Cinematography.
Msanii wa filamu Bongo, Monalisa ambaye binti yake Sonia Monalisa (19) kaanza muziki akiwa shule na mzazi wa mwigizaji maarufu, Mai Zumo (7) ambaye hivi karibuni naye kashinda tuzo, wameliambia gazeti hili kuwa ushindi wa Blue Ivy unatoa somo kwa wazazi kukuza vipaji vya watoto mapema.
Machi 15, 2021 Blue Ivy ambaye anatajwa kuwa mtoto maarufu zaidi duniani, alishinda tuzo ya Grammy katika kipengele cha Best Music Video na kumfanya kuwa mtoto wa pili mdogo zaidi kushinda tuzo hiyo.
Leah Peasall ambaye sasa ana miaka 29 ndiye anashikilia rekodi ya kuwa mtoto mdogo zaidi duniani kushinda Grammy mwaka 2002 akiwa na miaka minane.
Hata hivyo, Blue Ivy bado anashikilia rekodi ya mtoto mdogo zaidi kushinda tuzo ya Black Entertainment Television (BET) 2020 wakati huo akiwa na miaka minane kupitia wimbo huo huo (Brown Skin Girl).
Blue Ivy Carter ambaye baba yake ni Rapa Bilionea, Jay Z, alizaliwa Januari 7, 2021 katika Hospitali ya Lenox Hill, New York Marekani.
Beyonce alitangaza kuwa na ujauzito wa Blue Ivy Agosti 28, 2011 wakati akitumbuiza wimbo ‘Love on Top’ katika hafla ya utoaji wa tuzo za MTV Video Music Awards (VMAs) 2011.
Akizungumzia hilo, Habiba Zumo, ambaye mtoto wake Mai Zumo alishinda tuzo toka Mama’s Gala Awards kama Mtoto Mpambanaji katika Sanaa, anasema ni faraja na hatua nzuri kwa mzazi kuona mafanikio ya kipaji cha mtoto wake.
Anasema kubaini kipaji cha mtoto na kukipa nafasi ndio jambo la msingi zaidi.
“Hiyo ni changamoto kwa wazazi, wengi wao hawafahamu watoto wao ni vitu gani wanapenda, hivyo unakuta vipaji vyao vinapotea au hadi aje awe mkubwa ajue ndoto yake ni nini, pengine anakuwa ameshachelewa sana, lakini namshukuru Mungu tuligundua mapema na pengine sisi tupo kwenye tasnia ya uigizaji, basi ilikuwa rahisi sana kujua kipaji cha mtoto,” anasema Habiba.
Mai ambaye sasa anasoma darasa la pili, mama yake anasema waliweza kugundua kipaji chake kutokana na kuonyesha uwezo wa kukariri vitu kama matangazo kwenye runinga, jambo ambalo ndilo hasa linawapa wepesi kuigiza naye.
“Alianza kuigiza akiwa na umri wa miaka mitatu, alikuwa ni mtu wa kuiga vitu na kukariri kama matangazo na nyimbo, anaweza kusikia kitu kwa siku moja na akakirudia vilevile. Ana uwezo mkubwa wa kukariri, hiyo ndio imetusaidia kwenye uigizaji,” anasema Habiba.
Kwa upande wake Monalisa, akizungumzia ushindi wa Blue Ivy, anasema ndio kiu hasa ya mzazi kuona mtoto aliyemshika mkono katika sanaa yake anapata mapokezi na kazi yake kutambulika.
“Ni kitu kizuri kama mzazi, ukiona mtoto wako umemsaidia kufanya kitu kikaonekana na watu wakakipokea na wakampongeza kwa kile anachokifanya, ndio ndoto ya wazazi wote. Ukimpeleka mtoto shule hata akiitwa kuimba ngonjera pale mbele mzazi unajisikia vizuri, akiitwa ni mwanafunzi bora unajisikia vizuri, na ndicho tunachokitaka kwa watoto wetu, tuone mafanikio na maendeleo,” anasema Monalisa.
Pia, anasema yeye ni mzazi ambaye anaamini kwenye kipaji na elimu, ndiyo maana hata watoto wake wote anajitahidi kukuza vipaji vyao kwa kuwa ulimwengu unavyoendelea sasa hivi kipaji ni kitu kikubwa sana kutokana na watu wengi wamefanikiwa maishani kwa vipaji vyao.
“Ni muhimu kuwafunza watoto wakiwa wadogo, lakini sio tusubiri hadi wamekuwa wakubwa au wamemaliza vyuo ndio uanze kukuza hicho kipaji, unakuwa umechelewa, dunia ya sasa hivi inaenda mbio.
“Kiukweli ni kitu cha kumshukuru Mungu kwamba mtoto wako amepewa kipaji fulani na kama tayari una platform ni vizuri kumsaidia, labda tu kama hataki. Anajua kuimba lakini hataki kuwa mwanamuziki, usimlazimishe, kwa sababu wazazi hatutakiwi tuwalazimishe watoto kile kitu tunachokitaka sisi,” anasema Monalisa.
Pia, anasema sio kwamba mzazi ni daktari basi na mtoto lazima awe daktari, hapana! Kama anataka kuwa mhasibu aachwe asome na asaidiwe kutimize ndoto yake. “Kwa hiyo kama mzazi ni mwanamuziki na mtoto wake anajua kuimba, sio lazima na yeye awe mwanamuziki, bali aulizwe kwanza kama anavutiwa upande huo na sio kumlazimisha.”
Mtoto wa Monalisa, Sonia ambaye sasa anajiandaa kujiunga na masomo ya Chuo Kikuu, tayari ameachia nyimbo zake kama Umeenda na BYE, huku akifanya cover za wimbo wa Incase You Don’t Know wa Jux, Bado Kidogo wa Ben Pol na nyinginezo.
Akizungumzia hilo, mwimbaji wa taarabu, Khadija Kopa anasema hakuanza kukuza kipaji cha Zuchu tu, bali hata kwa marehemu mwanawe, Omari Kopa.
Anasema mtoto anapoonyesha kiu ya kufanya kitu fulani kinapaswa kuendelezwa na anapofanikiwa ni heshima kwa mzazi na kwake pia.
“Furaha iliyoje kijana au binti yako anapofanya vizuri katika kitu alichokuwa anakiota siku zote, mimi binafsi ninafurahi sana hilo likitokea.
“Watu wanaona sanaa inawaharibu watoto, lakini wapo walioharibikia ofisini, viwandani na shuleni, hiyo ni tabia ya mtu. Kama unavyosema mtoto wa Beyonce anapata tuzo kubwa, ina maana ataanza kujisomesha na kufanya vitu vyake vya msingi kupitia pesa yake mwenyewe, lakini atafungua milango mingine ya mafanikio, ikiwamo matangazo na ubalozi kwa sababu ameshakuwa na jina na haya ndiyo mafanikio ya sanaa,” anasema Khadija, ambaye mwanawe ni mwimbaji mahiri wa kundi la WCB, Zuhura Othmani, maarufu Zuchu anayetamba an nyimbo ‘Sukari’, ‘Nyumba ndogo’ na nyinginezo.
0 Comments