MSAADA PEKEE WA WAKULIMA NI KUONGEZA VIWANDA-MKENDA

Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda amemwambia Balozi wa Marekani nchini Dkt. Donald Wright kuwa Wakulima wa Tanzania wanahitaji uhakika wa masoko ya mazao ya kilimo pamoja na ujenzi wa viwanda vya kusindika na kuongeza thamani mazao ya kilimo kutoka kwa Wawekezaji wa nchini Marekani na kwamba Wizara ipo tayari kuratibu mkutano na Wafanyabiashara na wenye viwanda kutoka Marekani ili waje nchini kwa ajili ya kuwekeza kwenye Sekta ya Kilimo.

Waziri Mkenda amemueleza Balozi Dkt. Wright tarehe 16 Juni ofisini kwake Jijini Dodoma kuwa Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imefanya juhudi za makusudi kuhakikisha kilimo cha Tanzania kinakuwa chenye tija zaidi na cha kumuinua Mkulima.

Waziri Mkenda ameongeza kuwa bajeti ya Sekta ya Kilimo kwenye eneo la uzalishaji wa mbegu bora za alizeti imeongezeka mara dufu ili kuongeza uzalishaji wa alizeti kama njia mojawapo ya kupunguza uagizaji wa mafuta kutoka nje ya nchi ambapo taifa hutumia zaidi ya shilingi bilioni 474 kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi.

Waziri Mkenda alisema Wizara ya Kilimo imeweka mikakati mbalimbali ya kuongeza uzalishaji na tija kwenye mazao ya mafuta. Mikakati hiyo ni pamoja na kuongeza upatikanaji wa mbegu bora za mazao ya mafuta.

“Katika mwaka 2021/2022 Serikali imeongeza bajeti ya Taasisi ya Utafiti Tanzania (TARI) kutoka shilingi bilioni 7 mwaka 2020/2021 hadi Shilingi bilioni 11 mwaka 2021/2022 sambamba na hilo bajeti ya Wakala wa Mbegu wa Kilimo (ASA) imeongezeka kutoka bilioni 5 mwaka 2020/2021 hadi shilingi bilioni 10 mwaka 2021/2022 ili kuongeza upatikanaji wa mbegu bora zikiwemo mbegu za mazao ya mafuta.” Amekaririwa Prof. Mkenda.

No comments