HALMASHAURI MBOGWE WAPEWA SIKU TATU KUJIELEZA
Uongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbogwe iliyopo mkoani Geita umepewa siku tatu ya kutoa maelezo ya kwa nini usichukuliwe hatua kwa kushindwa kusimamia kikamilifu ujenzi wa mabweni mawili ya wanafunzi katika shule ya sekondari ya Lulembela licha ya kupewa shilingi milioni 150 miaka miwili iliyopita.
Agizo hilo limetolewa jana na Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia elimu Mhe.David Silinde wakati wa ziara yake ya siku moja wilayani humo ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo.
Mhe Silinde amewataka viongozi hao ambao ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Afisa Elimu Sekondari pamoja na Mkuu wa Shule hiyo Mwalimu Ernest Mganga kuhakikisha kuwa ifikapo jumanne wiki ijayo wanamwandikia maelezo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI sababu zilizopelekea ujenzi huo kutokamilika kwa zaidi ya miaka miwili baada ya kupokea fedha za ujenzi.
Amekifananisha kitendo hicho sawa na hujuma kwa viongozi wakuu wa nchi kwani kutokamilika kwa mabweni hayo kumesabisha serikali kushindwa kupeleka wanafunzi wa kidato cha tano mwaka huu.
“Miongoni mwa shule tulizopanga kuleta watoto wa kidato cha tano na sita mwaka huu ni shule yenu ya Lulembela, nakuja nakuta hali ni kama hivi, kwa hiyo inabidi niende nikazuie si ndiyo maana yake,” amesema Mhe.Silinde na kuongeza:
“Hapa maana yake DC hafanyi kazi, Mkurugenzi hafanyi kazi, Afisa Elimu Sekondari hafanyi kazi maana yake wote ni wazembe na kama mlimhujumu hayati Dkt John Pombe Magufuli maana yake mnamhujumu na Rais wa awamu ya sita.”
Naibu Waziri amewataka viongozi wa halmashauri hiyo kuwa wabunifu na kuhakikisha wanakamilisha mabweni hayo mapema iwezekanavyo ili yaweze kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa na serikali.
Pia ameonya kuwa hatosita kuchukua hatua dhidi ya viongozi hao endapo majengo hayo hayatakamilika mapema.
Awali Mkuu wa shule ya sekondari ya Lulembela Mwalimu Ernest Mganga akitoa maelezo ya ujenzi huo amesema kuwa yalijengwa mabweni mawili kila moja liligharimu kiasi cha shilingi milioni 75 changamoto iliyopo ni fedha kiasi cha shilingi milioni 150 kwisha kabla ya mabweni hayo kukamilika.
Post a Comment